October 21, 2016




Na Saleh Ally
SAKATA la Yanga kukodishwa bado linaendelea kutumika vibaya huku ikionekana waziwazi kwamba kuna maslahi ya watu ambao hawataki tu, ili mradi kutimiza matakwa yao.

Yanga ambao ndiyo wamiliki na wanachama ambao wameamua kukubali anayewekeza ndani ya klabu yao kwa kukodi timu na nembo afanye hivyo, bado inaonekana kuna ambao hawataki na huenda wana madaraka kusema hapana na ikawa na nguvu kuliko hata wanachama wenyewe wa Yanga.

Wanachama wa Yanga ndiyo wamekuwa wakisumbuka na Yanga kwa kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa. Mfano, kuitetea inapoonekana kuna anayetaka kuiyumbisha, kuwarekebisha wanaoonekana wanapotoka lakini lengo ni kuona kuna maendeleo.

Safari hii, suala la uwekezaji wa miaka 10 ambao ni maarufu kama ukodishwaji, linaonekana kuwa jambo lililowafanya hadi wale ambao hawakuwahi kusaidia lolote ndani ya Yanga kusimama na kutaka hilo lisifanikiwe.
Keshokutwa Jumapili wanakutana kwenye mkutano mwingine wa dharura, unaoweza kuamua hatima ya hilo.

Wanaokataa kinachoendelea hakuna wanaoweka wazi zaidi ya kusema utaratibu ufuatwe, wakati uongozi wa Yanga umeamua kuwaita wanachama wake na kulijadili suala hilo, wao wamesikika wanasema mkutano huo ni batili.

Maana yake wanaokutana tena ni batili, tena ikiwezekana hata wakiwa Wanayanga wengi mara mia zaidi ya wale wanaosema, bado itaonekana ni batili pia.

Inawezekana vipi sauti ya wengi ionekane haifai na sauti ya wachache ndiyo yenye nguvu zaidi? Hawa wachache wanapewa nguvu na nani hadi kufikia kuzuia kila wanachotaka wengi wakiamini ni sahihi?

Nani anayeweza kusema Yanga wote waliopitisha suala la huo ukodishwaji hawajui kitu? Lakini hao wanaojua vipi hawachambui kitaalamu hasara na faida, zaidi ya kuzungumza mambo kama “Manji aende zake”, “Ametukuta atatuacha”, “Sisi ndiyo wenye Yanga” na kadhalika?

Wapo wanaosema serikali haitaki, hofu ni kuwa mkodishaji atakuwa na nguvu sana. Huenda wanataka kuipaka matope serikali ambayo haiwezi kufanya jambo kama hilo. Nguvu ya Manji akikodisha timu, itakuwa kubwa kuliko ya serikali?

Kama hivyo ni kweli, maana yake hakutakuwa na mabadiliko katika mchezo wa soka milele. Maana ikifikia siku suala la uwekezaji, serikali itaogopa tena na kuona atakayetoa fedha zake atakuwa na nguvu, ninaamini Serikali ya Tanzania inahitaji maendeleo michezoni na sidhani kama inaweza kuwa na sababu nyepesi kama hizo.

Kama kuna sababu za hivyo, basi pia kuna haja ya kuangalia dunia tuliyopo na mwendo wa michezo yetu. Hakika fedha inahitajika kuleta mabadiliko. Sasa unataka mwenye fedha awe hana kitu kama Saleh Ally?

Kiasi ni mwenendo unaoshangaza, maana hata wale wanaojaribu kufafanua kuhusiana na mjadala huo, utasikia “watu wa Manji”! Lakini wanaopinga wanaona wao wana haki ya kuzungumza hata bila pointi za msingi na watakuwa sahihi. Hivi hawa ni watu wa nani?
Vizuri watu wawe huru kama ilivyo kwa wakosoaji. Kama BMT imetaka utaratibu ufuatwe basi ifanyike hivyo na kusiwe na figisu ya kukwamisha suala hili. Badala yake miongozo iwekwe, utaratibu ufuatwe, mwisho soka ipige hatua kwa kuangalia njia nyingine.
Mnaotetea maslahi yenu, mfano wenye mfarakano na Manji sijui mlinyimwa fedha za waganga, mlioshindwa kuwa watendaji sahihi akawatimua kazi, aliowanyima fedha za ubunge za kampeni, tofauti zenu zisiwe kwenye ishu ya Yanga, vizuri mkamvaa Manji binafsi na kupambana naye huko.

Zile taarifa watu wamepanga kuvuruga mkutano wa wanachama Jumapili, nazo si njema sana kwa kweli. Vizuri mkakumbuka mkutano huo utashirikisha babu na bibi zetu, hivyo onyesheni nidhamu na mjadili mambo yenu kwa busara, ikiwezekana iwe, ikishindikana pia si vibaya lakini itakuwa bora zaidi mkimaliza kwa amani, halafu litakalokuwa sahihi, basi ndiyo liendelee na maisha yaendelee kwa amani kama ilivyozoeleka ndani ya Tanzania yetu.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic