October 21, 2016


Muda mfupi baada ya gazeti la Championi kuandika taarifa kuwa Yanga ipo hatarini kupokonywa pointi nne kutokana na kumtumia beki Hassan Kessy wakati kesi yake ya usajili ikiwa haijamalizika, haraka sana Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limemtafuta mjumbe wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kulishughulikia suala hilo.

Kessy ambaye ametua Yanga msimu huu akitokea Simba, amesababisha mvutano baina ya pande mbili za timu hizo na mpaka sasa hatua iliyokuwa ni kuwa klabu hizo zinatakiwa kukutana pamoja kufikia muafaka kiungwana kabla Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF haijatoa maamuzi yake.

Awali, kulikuwa na makubaliano kuwa Yanga na Simba zikutane chini ya mjumbe wa zamani wa TFF ambaye pia ni Mjumbe wa Heshima wa Caf, Said El Maamry aliyependekezwa na klabu hizo pamoja na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF lakini El Maamry alikuwa hajapewa taarifa hizo hadi kufikia juzi.

El Maamry alisema baada ya gazeti hilo kutoa taarifa juu ya Yanga kuwa na uwezekano wa kupokwa pointi ndipo alipopokea barua ya maombi ya kuitwa kwa ajili ya suala hilo.

“Nimeipata barua jana (juzi, hiyo ilikuwa ni baada ya kusoma katika Gazeti la Championi, pamoja na hivyo sijajua ni lini nitakutana na pande hizo mbili kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.

“Kwa sasa siwezi sema chochote mpaka hapo nitakapokuwa nimekutana na viongozi hao ambao naweza kusema wameamua kunichagua mimi kuwa msuluhishi wao kwa sababu ya ufahamu wangu mkubwa wa sheria na mambo mbalimbali ya soka,” alisema El Maamry ambaye pia hakutaka kuweka wazi ambacho kinaweza kuikumba Yanga kama muafaka wa suala hilo hautafikiwa.

Alipotafutwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sheria na Uanachama ya TFF, Elliud Mvela hakupatikana lakini upande wa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, alisema: “Sisi tulishatoa maamuzi yetu lakini tukawaambia kuwa wamalizane kwa njia ya usuluhishi, endapo watashindwa kufikia makubaliano, tutarejea katika maamuzi yetu tuliyokuwa tumefikia hapo awali.

“Kuhusu suala ya Yanga kuendelea kumtumia Kessy katika mechi zake hilo naomba tuliache kwa sasa wakati pande hizo mbili zikiwa kwenye mazungumzo.”

Upande wa Msemaji wa TFF, Alfred Lucas, alisema: “Kesi ya msingi iliyopo kwao ni Simba kudai fidia ya Kessy kukiuka mkataba wake, hakuna sehemu walikoonyesha kupinga usajili wake kwenda Yanga, hivyo kiusajili Kessy ni halali Jangwani.

“Simba wao waliainisha kuwa walipwe dola laki sita (Sh bilioni 1.3) kama kipengele cha mkataba wake kilivyoainisha. Hivyo ishu ni uvunjwaji wa mkataba na siyo ishu ya usajili wake kwenda Yanga.

“TFF iliagiza wakutane wayamalize, Simba walimteua Said El Maamry wakati Yanga wakamteua Nondo Fimbo."

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic