October 21, 2016


KICHUYA

Winga wa Simba, Shiza Kichuya ambaye kwa sasa ndiye gumzo kubwa katika mitaa mbalimbali hapa nchini kutokana na uwezo wake mkubwa anaouonyesha uwanjani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar, ametoa tamko kuhusu baba yake mzazi, Ramadhani Yahaya Kichuya ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga.

Kichuya amefunguka kuhusu baba yake ambaye wiki kadhaa zilizopita alisema kuwa aliumia kuona mwanaye akifunga bao dhidi ya Yanga kwa kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Yanga lakini hakuwa na jinsi kwa kuwa mwanaye alikuwa kazini.

Bao hilo alifunga wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam likiwa ni la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 1-1.

Kichuya mdogo anasema: “Siku hiyo baba yangu aliumia sana kwa sababu ni shabiki mkubwa Yanga lakini kwa upande wangu sikuwa na jinsi kwani ilibidi nifunge kwa ajili ya mafanikio ya timu yangu ya Simba ambayo ndiyo naifanyia kazi.

“Soka ndiyo kazi yangu na ninatakiwa kupambana kwa nguvu zangu zote ili kuhakikisha naisaidia timu yangu kupata mafanikio, nilijua kabisa nikiifunga Yanga mzee wangu ataumia sana kwa sababu ni shabiki mkubwa wa timu hiyo lakini siku wa jinsi.

“Hata hivyo namshukuru Mungu kwani mzee wangu naye analijua hilo, hivyo namuomba awe mvumilivu tu, aniache nifanye kazi yangu hata siku nyingine nitakapokutana na Yanga nitacheza kwa nguvu zangu zote na nikipata nafasi ya kufunga nitafunga.”

Kwa sasa Kichuya ndiye anayeongoza kwa kuzifumania nyavu katika michuano hiyo, ana mabao saba ambayo amefanikiwa kuyapata katika mechi tisa alizoitumikia timu hiyo tangu alipojiunga nayo hivi karibuni.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV