January 27, 2017



Na Saleh Ally
WAKATI mwingine unaweza kujiuliza kumbe wahusika wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanaweza kuwa wasikivu namna hii! Kwamba ni watu wanaoweza kushauriwa jambo fulani na mara moja wakalifanyia kazi?

Kawaida imekuwa ni kama ushindani, hata ushauri jambo zuri namna gani lakini kwa kuwa umeandika gazetini, basi hakuna kiongozi ambaye anaweza kukubali kulifanyia kazi jambo hilo kwa kuwa asingependa kuonekana amefundishwa na gazeti.


Kumekuwa kama kuna ushindani wa makusudi na kila anayekosolewa hasa katika mchezo wa soka, huona ameonewa au anataka kuharibiwa jambo fulani.


Karibu kila mwandishi ambaye anakosoa huonekana anatumika kumharibia kiongozi dili au mambo yake. Neno “unatumika” limekuwa ngao kwa kila anayekosolewa kwa kuwa kila mmoja hataki kuambiwa ukweli.


Lakini safari hii, Gazeti la Championi lilikuwa kati ya wadau wa mchezo wa soka lililolalamika kuhusiana na ubovu wa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro baada ya mechi ya Mtibwa Sugar dhidi ya Simba.


Mechi hiyo iliisha kwa suluhu lakini hakukuwa na burudani zaidi ya kichefuchefu cha mechi kuchezwa kwenye majaruba.


Gazeti hili lilieleza wazi kero hiyo, likaeleza namna ambavyo wahusika wa uwanja wasivyojali kwa kuwa wanaendelea kuingiza fedha, lakini TFF wakiwa wamejisahau nao bila ya kujali afya za wachezaji au fedha za mashabiki ambao wanalipa kuona burudani ya soka.
Wanakuja kuambulia karaha badala ya furaha na mateso ya moyo kwa kuwa hakuna burudani ya soka sababu ya uwanja waovyo kabisa.


Mwisho gazeti hili likatoa ushauri kwa TFF kuwa macho na wamiliki wa uwanja na ikiwezekana waufungie ili wasipopata fedha, wakumbuke kuukarabati. Wasipoufungia, wahusika wataendelea kuingiza fedha na wachezaji wakiendelea kuumia na mashabiki kuambulia karaha.


Siku mbili tu mbele, TFF na Bodi ya Ligi wamepitisha uamuzi wa kuufungia huo uwanja hadi hapo wamiliki Chama cha Mapinduzi (CCM) watakapoufanyia marekebisho katika sehemu ya kuchezea au “pitch”.


Hii imekuwa ni kawaida kabisa, kwa viwanja kutokuwa na viwango bora na wahusika hawalioni hili. CCM Mkoa wa Morogoro vipi? Kwani kipi hasa ambacho hawakioni katika hilo au wanafanya makusudi?


Kwa kuwa wanaingiza fedha na mifuko yao inaendelea kutuna basi hawaoni kama wana sababu ya kufanya ukarabati na kuboresha pitch kwa ajili ya afya ya wachezaji na burudani kwa wanaowaingizia fedha!


Kwangu naona ni aibu kwa CCM Morogoro, wanaonyesha kiasi gani hawapo makini. Kumiliki uwanja wa michezo bila ya pitch bora ni sawa na kumiliki trekta lisilokuwa na jembe. Hakuna manufaa na kama wanataka manufaa zaidi basi waugeuze uwe ukumbi wa disco.


Iko haja wamiliki kama CCM kuanza kutafakari kwamba wanatakiwa kuhakikisha viwanja vinakuwa na ubora kwa kuwa mabadiliko katika maisha ya michezo yamekuwa na kasi kubwa sana.


Kama uongozi wa CCM Morogoro umesimamia huo uwanja kwa miaka 10 iliyopita au zaidi, lazima ujue mwaka 2017, mambo ni tofauti na huenda hata 2016 walipita kibahati. Haiwezekani uwanja mkubwa kama wa Jamhuri ukawa na sehemu mbovu ya kuchezea unaolingana na viwanja vya kuchezea soka la mchangani.


Lazima ubadilishwe, wakishindwa wahusika basi waubinafsishe ili wajitokeze watu watakaouendesha. Awali niliwahi kuambiwa kuna viongozi wamekuwa wakipinga viwanja kubinafsishwa, hasa wale wa mikoani kwa kuwa nao hufaidika maana kuna mechi, matamasha na hata kodi za maduka yanayozunguka uwanja.


Kama yote hayo yanapatikana basi fedha zinaingia. Hivyo badala ya kuangalia faida zenu binafsi, basi ingizeni fedha kukarabati viwanja, dhamana ambayo mmekabidhiwa kwa kuwa si mali yenu binafsi.

Hongera TFF na Bodi ya Ligi kwa kubadilika, angalau kwa kuwa waungwana kidogo na kuweza kuwajali wanasoka wa Tanzania na mashabiki ambao wanatoa fedha zao na wanastahili burudani bora na sahihi.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic