August 11, 2017




Na Saleh Ally
UCHAGUZI wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) msimu huu nauona hauna tofauti kabisa na ule mwingine uliopita miaka minne iliyopita wakati Jamal Malinzi alipofanikiwa kumbwaga Athumani Nyamlani na kuibuka na ushindi.

Nyamlani alikuwa ni Makamu wa Rais wa TFF, lakini alibwagwa na Malinzi ambaye wadau wengi waliamini alikuwa amebaniwa sana na angekuwa chachu ya kuleta maendeleo katika shirikisho hilo.

Hakuna aliyekuwa akipinga juhudi za rais aliyekuwa akimaliza muda wake wakati huo, Leodegar Tenga, wazi alionekana kufanya mambo kadhaa ambayo yalionekana kuwa ni mabadiliko.

Kutoka Chama cha Soka Tanzania (Fat) kwenda TFF. Baada ya hapo alitakiwa mtu wa kuendeleza mambo na wote tunajua kwamba Tenga alitengeneza mfumo mzuri, watu kufanya kazi kwa kufuata mpangilio sahihi na mabadiliko tuliyaona.

 Utawala wa Malinzi ulitakiwa kufanya muendelezo, lakini ulipoingia tu ukafanya mambo ya ajabu kabisa, kwanza ilikuwa ni kuondoa kila aliyeonekana kuwa ni “mtu wa Tenga” ili kuweka watu wapya ambao wanaonekana ni “Watu wa Malinzi”.

Hakuna aliyefikiria kwamba wanachokikuta kilifanywa na watu hao waliowakuta madarakani na wangekuwa msaada mkubwa kwao kufanya mambo zaidi. 


Walioingia wengi tukawaona hawakuwa wamewahi kuongoza hata wilaya kisoka, wakapewa madaraka makubwa na kubandikwa jina la ushauri na ndiyo waliotufikisha hapa tulipo, wakiwa wameturudisha nyuma kwa asilimia kubwa kabisa.

Kipindi hiki nawaona kwa mara nyingine watu wakiendelea kupiga kampeni kwa ajili ya uchaguzi ujao ambao utafanyika Agosti 12, mwaka huu huko Dodoma. Utaona kila mgombea anapiga kampeni zenye maneno matamu.

Sitaki kuamini kampeni maana yake ni maneno ya uongo. Ninaamini wanaofanya kampeni ni watu wazima wenye akili zao na wanajua wanazungumza mbele ya umma. Na wanajua wanayoyazungumza hayatasahaulika na siku moja tutahoji.



Tumeona mengi ambayo uongozi wa Malinzi uliahidi kuyafanyia kazi umefeli na umekuwa mbogo ukiulizwa jambo hukumbushia machache uliyoyafanya.
Yale machache kabisa, mazuri waliyoyafanya, mara zote tumekuwa tukiyakumbushia kwa kuyazungumzia na kusema wanastahili angalau hiyo pongezi kidogo.

Lakini yale wanayofanya vibaya tunayakemea ingawa imekuwa vigumu wao kukubali kwa kuwa wanaona ni kero kubwa na uonevu kuambiwa ukweli. Huku baadhi waliowachagua kuwa “watumishi” wao wakiwatetea kwa kila linalotokea kwa kuwa wanafaidika na mambo kadhaa na si mpira wa Tanzania tena.

Sasa wanaopiga kampeni nao ni wanadamu kama ambao wametoka madarakani na wanajua kabisa kwamba kuna mambo mengi uongozi uliopita ulifeli.

Najua ili kufanya kampeni ni lazima kupitia kadhaa ambayo ni tatizo kutoka kwa uongozi uliomaliza muda wake madarakani. Watakuwa wameyaona na wao wameongeza ubunifu wao na nini hasa wanataka kufanya ili kutukwamua katika tope kutoka hapa tulipo. 

Kama wanajua na wanaona kila tulikopitia, ninaamini watakuwa ni watu wenye kauli thabiti na watakuwa ni watu ambao wanaamini wanawaambia yaani sisi na Watanzania wapenda soka na michezo kwa ujumla kuwa ni watu tunaojielewa na tunaelewa wanachoelezea.

Kati ya wagombea wanaopiga kampeni ni lazima wako watakaoshinda. Sasa nataka kuweka msisitizo kwa wagombea, kwamba atakayepata nafasi ya kuingia katika nafasi yoyote ile, nyimbo au kampeni wanazopiga wakitueleza, uwe ndiyo msingi.

Kampeni sawa, lakini utekelezaji ndiyo jambo sahihi zaidi na kitu ambacho tungependa kukiona kinafanyiwa kazi na mwisho kuwe na matunda ambayo yatazaa mabadiliko.
Tanzania ni nchi yetu sote, kusiwe na wale wanaotaka kutumia kitu cha umma kwa ajili ya kujifaidisha. Kusiwe na yule anayetaka kutudanganya halafu akipata nafasi anafanya anavyotaka yeye na kiburi juu. 
Kama kuna mtu anataka maendeleo na anataka kufanya anavyotaka yeye, basi aanzishe kampuni yake binafsi afanye anavyotaka badala ya kutudanganya kwa nyimbo zenye mvuto masikioni mwetu, mwisho wa siku, anatuburuza, anatudanganya na kufanya mambo ya kijinga yanayoturudisha nyuma. Watu wamechoka, fanyeni kampeni, mkipata nafasi kafanyieni utekelezaji mnayotuambia leo.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic