KOCHA wa timu ya Lipuli, Seleman Matola amesema kuwa bado ndani ya kikosi kwa upande wa uchumi haijakaa sawa ila wachezaji wake amewajenga kisaikolojia kubeba pointi tatu mbele ya Mbao.
Lipuli imepoteza pointi tisa mfululizo baada ya kuanza mbele ya Stand United Uwanja wa Kambarage wakafuata mbele ya Simba Uwanja wa Samora, kisha pointi tatu nyingine wakaziacha Kagera Sugar mchezo uliochezwa Uwanja wa Kaitaba.
Matola amesema kuwa wachezaji wake walikaa kikao na uongozi kisha wakazungumza kuhusu matatizo yao na wamefikia muafaka hivyo leo watapambana.
"Kwa sasa kikosi kina hali mbaya kiuchumi najua kabisa sina hela ila nimewajenga wachezaji wangu kupambana na tutabaki na matokeo kwenye Uwanja wa nyumbani hapa Samora.
Kocha wa Mbao, Ally Bushiri amesema wanatambua kwa sasa kila timu inahitaji pointi tatu hivyo nao mpango wao ni kubeba pointi tatu.
"Kila kitu kipo sawa ni suala la wakati tu, tunawaheshimu wapinzani wetu ila hamna namna tunahitaji pointi tatu," amesema Bushiri.
Kukosekana kwa mdhamini mkuu wa ligi kumezifanya timu nyingi kujiendesha kwa kuungaunga hali ambayo inapelekea wachezaji wengi kuwa na migomo ya kimyakimya ndani ya timu zao.








0 COMMENTS:
Post a Comment